Baada ya kushambuliwa kwa kejeli na
Rwanda, Rais Jakaya Kikwete amevunja ukimya na kueleza kushangazwa na
kauli hizo na maneno yasiyofaa yanayotolewa na viongozi wa nchi hiyo
dhidi yake na Tanzania.
Badala yake amesema Tanzania haina
mgogoro wowote na nchi hiyo wala haiwezi kufanya vitendo vyovyote vibaya
dhidi yake, nchi nyingine jirani au yoyote duniani, kwani migogoro
haina tija wala maslahi kwa Watanzania.
Rais Kikwete alieleza mshangao huo jana
katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi ya kuzungumza na taifa, na kusema
kuwa yeye binafsi na serikali ya Tanzania haina ugomvi wala nia yoyote
mbaya na Rwanda.
"Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa
Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika
uhusiano na ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile.
Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo
lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka
kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu," alisema na kuongeza:
"Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake.
Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa
aina yoyote. Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo.
Waingereza wanasema 'two wrongs do not make a right'.
Alikiri kuwa katika kipindi cha miezi
miwili uhusiano baina ya nchi hizo umekuwa ukipita katika kipindi kigumu
na kwamba kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yake na nchi ni ushahidi wa
hali hiyo.
"Napenda kuwasisitizia kuwa mimi na
serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo
vibaya dhidi ya Rwanda au nchi nyingine yoyote duniani.
Hatuna sababu ya kufanya hivyo, kwani mambo hayo hayana tija wala maslahi kwetu," alisema.
Rais Kikwete aliwahakikishia Watanzania
na Wanyarwanda kuwa, Tanzania inapenda kuwa na uhusiano na ushirikiano
wa karibu na Rwanda kama ilivyo uhusiano wake na nchi zingine jirani na
kuongeza kuwa kama majirani kila mmoja anamhitaji mwenzake, hivyo lazima
uwepo uhusiano mwema.
Kwa mujibu wa Rais, wakati Tanzania
imekuwa ikijihusisha siku zote na kukuza na kujenga ujirani mwema,
kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano kwa maslahi ya nchi
zote mbili na kwamba hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje
ya Tanzania kabla na baada ya kutokea sintofahamu.
Alisema Rwanda na Tanzania zimekuwa na
uhusiano mzuri miaka mingi, zikishirikiana na kusaidiana katika mambo
mengi kitaifa, katika kanda ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu,
Umoja wa Afrika na hata kimataifa, hata hivyo mtikisiko huo umekuja
baada ya kutoa ushauri kwa serikali ya Rwanda kufanya mazungumzo na
mahasimu wao.
"Nilitoa ushauri ule kwa nia njema
kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya
mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa
pia kwa Serikali ya Kongo (DRC) na kwa Serikali ya Uganda.
Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni
wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema chochote
pale mkutanoni lakini baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia
maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia," alisema.
Rais Kikwete alisema anastaajabu jinsi
Rwanda ilivyouchukulia ushauri wake na haufanani na wanayoyafanya, huku
akisisitiza kuwa alifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi za miaka
mingi katika ukanda huo.
Alisema ni kawaida kukutana katika
mikutano na vikao mbalimbali kuzungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya
njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea na
kwamba wakati waliyachukulia kuwa ni mambo yanayohusu wote, hivyo
kupeana ushauri ni wajibu wa wote.
"Mara nyingi ushauri kwa wanaogombana
kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane
jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa!
Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si
shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa.
Muungwana hujibu: "Siuafiki ushauri wako". Hakuna haja ya kutukana
wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo,"
alisema.
Alisisitiza Tanzania inapenda kuendelea
na uhusiano mzuri na Rwanda na kuongeza kuwa labda kama Rwanda ina jambo
dhidi ya Tanzania, kwa kile alichosema kusikia mengi yanayozungumzwa na
kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yake na nchi. Hata hivyo,
alisema hapendi kuyaamini hayo yanayosemwa moja kwa moja lakini pia kama
nchi hawatayapuuza.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete
alisema kauli yake aliyoitoa katika Sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa
ilitafsiriwa vibaya na kwamba hakutaja mtu wala nchi yoyote bali
alizungumzia wajibu wa majeshi na raia kulinda uhuru na mipaka ya nchi.
Rais Kikwete alisema hataruhusu mtu au
nchi yoyote kupokonya wala kuichezea haki ya Watanzania hiyo na
kusisitiza utayari wa nchi kulinda mipaka yake, huku akitoa mfano wa
mashujaa waliofariki dunia kwa kulinda nchi kuwa ni fundisho kwa mtu
yeyote anayetamani kumega kipande chochote cha ardhi ya nchi ya
Tanzania.
Baada ya kutoa kauli hiyo baadhi ya
vyombo vya habari vilitafsiri kauli hiyo kuwa amewasema Malawi na Rwanda
kutokana na kuwepo sintofahamu na viongozi wa nchi hiyo. Malawi na
Tanzania wanagombea mpaka wa Ziwa Nyasa.
Alisisitiza kauli yake ya awali
aliyoitoa mkoani Kagera ya kuwapa siku 14 wale wanaohusika na ujambazi,
uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua
muafaka sasa, badala ya kusubiri operesheni iwakute, wala wasifikirie
kuwa hili ni jambo la kupita.
Pia alizungumzia ziara za viongozi wa
mataifa mbalimbali akiwemo Rais wa Marekani, Barack Obama ambapo alisema
ziara ya kiongozi huyo imeimarisha uhusiano mzuri baina ya mataifa
mbalimbali pamoja na kutoa fursa na miradi mbalimbali kwa ajili ya
maendeleo ya Watanzania.
Alisema katika ziara hiyo, Rais Obama
pia alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza
ushirikiano wa biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ameielekeza Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kutengeneza
mkakati utakaoonesha jinsi watakavyojipanga kufaidika na mpango huo.
Alitaja viongozi wengine ambao walifanya
ziara hapa nchini kuwa ni Rais Mstaafu wa Marekani, George W Bush,
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na Waziri Mkuu wa
Thailand, Yingluck Shinawatra, ambapo ziara za viongozi hao wote
zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada za Tanzania kujiletea
maendeleo.
No comments:
Post a Comment