London, England.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ameendelea kufanya mabadiliko katika kikosi chake baada ya juzi kumsajili winga Mohamed Salah kutoka klabu ya Basel.
Taarifa ya klabu ya Chelsea ilisema, “Klabu ya
Chelsea inaweza kuthibitisha kwamba tumekubaliana na klabu ya FC Basel
na tutamchukua kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mohamed Salah.”
Kutokana na makubaliano hayo, klabu ya Chelsea
inatarajiwa kumtambulisha Salah siku ya Jumapili wakati Chelsea
itakapokuwa ikicheza na Stoke mechi ya Kombe la FA raundi ya nne.
Salah atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na
Chelsea katika kipindi hiki kwani tayari imewasajili wachezaji Betrand
Traore na Nemanja Matic. Wachezaji hao wamesajiliwa na Chelsea baada ya
kuwauza nyota Kevin De Bruyne na Juan Mata.
Mourinho amemsajili Salah kwa sababu anaona ni
mchezaji mbadala anayeweza kuziba pengo la Mata aliyeuzwa katika klabu
ya Manchetser United.
Hata hivyo, usajili huo wa Mata kwenda Manchester
United umeonekana kumshangaza sana kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kwani
alisema Chelsea haitaathirika kwa kumuuza Mata ila timu nyingine ndiyo
zitaathirika.
Wenger alisema Chelsea wameishacheza na Manchester
United nyumbani na ugenini msimu huu kwa hiyo hawataathirika kwa
kumuuza Mata.
“Mimi nadhani kipindi hiki cha usajili wa dirisha
dogo kingesimamishwa wakati timu zikiwa zimeishakutana mara moja na
kumalizika mzunguko wa kwanza,”alisema Wenger.
Kocha Wenger alikanusha taarifa zilizopo kwamba
anataka kumsajili mshambuliaji wa Barcelona Cristian Tello kwani
alikwenda Hispania kushuhudia mechi kati ya Barcelona dhidi ya Levante.
Hata hivyo, zipo taarifa kwamba Arsenal bado
inaendelea na harakati zake za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Schalke,
Julian Draxler kwa ajili ya kuziba pengo la mshambuliaji wake Theo
Walcott aliyeumia goti.
No comments:
Post a Comment